Makala haya yanachunguza ngazi ya itikadi na uamilifu wake katika riwaya teule za Kiswahili kupitia kwa ufokasi. Riwaya teule ni Haini (Adam Shafi, 2003), Makuadi wa Soko Huria (C. Chachage, 2005), Harufu ya Mapera (K. Wamitila, 2012), Hujafa Hujaumbika (F. Kagwa, 2018), Ndoto ya Almasi (Ken Walibora, 2006) na Nyuso za Mwanamke (S. Mohamed, 2010). Ngazi ya itikadi ni mojawapo ya ngazi mbalimbali za ufokasi zilizopendekezwa na wananaratolojia. Kimsingi, ufokasi ni mkabala ambao huchukuliwa katika kuwasilisha simulizi na kuikuza hadithi kwa ujumla. Data ya kuudhibiti na kuthibitisha madai ya mjadala wetu imetolewa katika riwaya teule. Uteuzi wa riwaya hizi unahalalishwa kwa misingi kwamba, hizi ni riwaya zilizo na matini pana zinazowezesha udondoaji wa mifano faafu inayodhihirisha ngazi ya itikadi na wakati huo huo kudhihirisha uamili wa ngazi hiyo katika simulizi. Mjadala wa kimsingi katika makala haya umekitwa na kuongozwa na teneti za kimsingi za nadharia ya naratolojia ambayo inatambua ufokasi kama kipengele muhimu katika uwasilishaji wa simulizi. Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa, kupitia kwa ufokasi nje na ndani, waandishi wa riwaya teule wamedhihirisha ngazi ya itikadi. Imebainika kuwa wahusika mbalimbali huwa na tabia, mitazamo, misimamo na hisia fulani kuhusu masuala mbalimbali kutokana na athari za itikadi zinazotawala mazingira au matamanio yao